Jinsi ya kuandika CV nchini Kenya (na mifano)
CV nyingi nchini Kenya husomwa kwa chini ya dakika moja, mara nyingi kwenye simu, na mtu aliye na CV nyingine 200 za kusoma. Lengo ni moja: kumrahisishia akupigie simu. Mwongozo huu unapitia kila sehemu, na mifano ya mstari dhaifu na mstari wenye nguvu.
1. Jina na mawasiliano
Jina lako kamili kwa herufi kubwa, kisha kwenye mstari mmoja: nambari ya simu yenye tarakimu 10, barua pepe unayoangalia kila siku, na mji unaoishi. Inatosha.
| Dhaifu | Bora |
|---|---|
| Simu: 712 34 567 | 0712 345 678 |
| P.O. Box 1234, Nyumba Na. 14, Kahawa West | Nairobi (Kahawa West) |
Tarakimu moja ikikosekana, mwajiri hawezi kukupigia. Soma nambari yako kwa sauti kabla ya kutuma.
2. Kazi unayotaka na maelezo mafupi
Chini ya jina lako, andika kazi unayotafuta: Cashier, Dereva (BCE), Msaidizi wa Ofisi. Kisha mistari miwili au mitatu: unafanya kazi gani, kwa muda gani, jambo moja ulilofanikisha, na kazi unayotaka.
| Dhaifu | Bora |
|---|---|
| Mimi ni mchapakazi, mcha Mungu na ninapenda kufanya kazi na wengine. | Cashier mwenye uzoefu wa miaka 3 katika supermarket yenye shughuli nyingi Thika. Nimesawazisha till bila upungufu karibu kila zamu na nimewafunza cashier wapya 3. |
Maneno kama "mchapakazi" yako kwenye karibu kila CV, kwa hivyo waajiri huyaruka. Dini haifai kuwa kwenye CV.
3. Uzoefu wa kazi
Anza na kazi ya karibuni zaidi. Kwa kila kazi: cheo, mwajiri, mji, na mwezi na mwaka ulioanza na kumaliza. Kisha mambo 2 hadi 4 uliyofanya. Kila jambo lianze na kitenzi cha kitendo, na liseme ni kiasi gani au wangapi pale unapoweza.
| Dhaifu | Bora |
|---|---|
| Nilihusika na wateja. | Served about 80 customers a day at the main till. |
| Kazi zangu zilikuwa kushughulikia pesa. | Handled cash and M-Pesa payments of around KES 150,000 a day with no shortages. |
CV nyingi nchini Kenya huandikwa kwa Kiingereza, kwa hivyo mifano ya safu ya pili iko kwa Kiingereza. Attachment, internship, kazi za kibarua, kujitolea na biashara yako mwenyewe zote ni uzoefu. Ziandike kwa njia hiyo hiyo.
Tarehe: andika mwezi na mwaka, kwa mfano Mar 2022 – Aug 2024. Ukiwa na pengo la zaidi ya miezi 6, ongeza mstari mmoja wa ukweli: kozi, majukumu ya familia, biashara ndogo au kutafuta kazi.
4. Elimu
Anza na ya juu zaidi. Kozi, chuo, mwaka uliomaliza na alama. Weka alama yako ya wastani ya KCSE, kwa sababu matangazo mengi huweka kiwango cha chini (kwa mfano C- na zaidi). Ukishakuwa na KCSE, huhitaji kuandika KCPE.
5. Ujuzi
Ujuzi 5 hadi 8 unaolingana na kazi unazotaka, kwa maneno ambayo matangazo hutumia: cash handling, M-Pesa, customer care, MS Excel, driving licence BCE. Usiweke asilimia au nyota ("Excel 80%"). Hazimwambii mwajiri chochote.
6. Wadhamini (referees)
Watatu, kila mmoja na cheo chake, mahali anapofanya kazi, na nambari ya simu anayojibu. Waombe ruhusa kwanza. Wanafunzi: mhadhiri au msimamizi wako wa attachment anafaa.
Usiweke haya kwenye CV
- Nambari ya kitambulisho, pasipoti au tarehe ya kuzaliwa. Mwajiri huomba haya baada ya kukuajiri.
- Hali ya ndoa, dini, kabila, na kijiji au kaunti ya nyumbani.
- Anwani kamili ya nyumbani. Mji unatosha.
- Picha, isipokuwa tangazo limeiomba.
- "Referees available on request".
Urefu na muundo
Ukurasa mmoja au miwili. Tuma kama PDF isipokuwa tangazo limeomba Word, na uipe faili jina lako, kama mercy-wanjiru-CV.pdf. Kabla ya kutuma, isome kwa sauti mara moja. Waajiri wengi huacha kusoma wanapoona kosa la kwanza la tahajia.
Bure. Huhitaji kujisajili. Tunakuonyesha cha kurekebisha na kazi zinazokufaa.
Angalia CV yangu bure